Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar

MASHEHA NA MADIWANI WASISITIZWA KUFUATA MAADILI – DC.

Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘B’, Hamid Seif Said, amesema ipo haja kwa kila Kiongozi wa Umma kukamilisha taratibu zilizowekwa naTume ya Maadili  hasa katika suala la kujaza fomu za maadili.

Mkuu huyo alisema hayo wakati akifungua mkutano wa siku moja uliofanyika katika Ukumbi wa Baraza la Mji Kaskazini “B” uliowakutanisha Masheha na Madiwani wa Wilaya ya Kaskazini ”B” Unguja.

Alisema katika kazi zote zinazofanywa na viongozi ni lazima kila mmoja   ahakikishe   anatimiza wajibu wake   sambamba na kusimamia maadili katika majukumu yao ya kazi na hata kwa jamii.

Aidha aliwataka Viongozi hao  kuhakikisha kila mmoja anajaza fomu hizo kwa usahihi ili kuisaidia Serikali kujua uhalali wa umiliki wa mali za viongozi hao na  pia kuwa  kigezo kwenye  jamii  katika kufuata maadili kwa vitendo.

“Wapo viongozi ambao tayari washajaza fomu hizo awali lakini kiutaratibu kila ifikapo mwisho wa mwaka viongozi wanatakiwa wajaze fomu hizo”, alisisitiza.

Abdul-latif Ally Ally, Afisa Usajili kutoka Tume ya Maadili  akiwasilisha mada juu ya Uhakiki wa taarifa za Tamko la Mali na Madeni kwa Viongozi wa Umma, alisema ni muhimu kwa Viongozi wa Umma kujua namna Tume ya Maadilii inavyoshughulikia malalamiko    ya uvunjwaji wa Maadili kwa Viongozi na hatua zinazochukuliwa.

Kwa upande wa Mkuu wa Kitengo cha Habari kutoka Tume hiyo, Halima Jumbe Said alisema Tume imepewa mamlaka ya kupokea na kusajili Tamko la Rasilimali na Madeni kwa kila kiongozi wa umma aliyetajwa katika Jadweli la kwanza la Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma nambari 4 ya mwaka 2015.

Alisema kuwa Sheria hiyo inaelekeza kuwa kila kiongozi anapaswa kufuata miongozo  na  taratibu za kujaza fomu ili kufanyiwa uhakiki wa taarifa zilizomo katika fomu hizo.

Alisema wapo baadhi ya Viongozi huficha mali na mapato yao wakati wa kujaza fomu za Tamko  jambo ambalo ni kinyume na Maadili kwa mujibu wa Sheria.

Alifahamisha kuwa kukosekana kwa taarifa za wenza wao katika fomu ni miongoni mwa changamoto zinazopelekea kutopata taarifa sahihi za uhakiki huo.

Aliongeza kuwa iwapo Tume haikuridhika na taarifa zilozowasilishwa na Kiongozi wakati wa uhakiki hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake kama sheria inavyoelekeza.

Kwa upande wa Masheha na Madiwani waliipongeza Tume ya Maadili  kwa kuwa na utaratibu mzuri wa kutoa elimu kwa viongozi wa Umma wenye lengo la kuwakumbusha umuhimu wa kukuza Maadili katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.