Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar

Tume ya Maadili yatayarisha Mkataba wa Huduma kwa wateja kukidhi mahitaji ya wananchi

KATIBU wa Tume ya Maadili ya viongozi wa Umma, Asma Hamid Jidawy, amewataka watumishi wa umma kutumia nafasi zao na taaluma zao ili kuweza kukemea maovu na kutoa taarifa za uvunjifu wa maadili kwa viongozi wa umma.

Akifungua mkutano wa siku moja wa kujadili rasimu ya mkataba wa huduma kwa wateja kwa niaba ya Mwenyekiti wa Tume hiyo, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano ZSSF Kariakoo mjini Unguja amesema kuwa watumishi endapo watatumia nafasi zao kutoa taarifa kutaiwezesha jamii kuepuka matatizo mbali mbali ambayo mengine yangaliweza kuzuilika kabla ya kuathiri jamii na Serikali.

Alifafanua kuwa lengo la kuandaa mkutano huo ni kupokea maoni juu ya rasimu ya mkataba wa huduma kwa wateja ili kuweza kutumika na kurahisisha upatikanaji wa huduma baina ya wananchi, viongozi na Tume hiyo.

Sambamba na hayo, aliongezea kuwa rasimu ya mkataba huo pia itawezesha kutoa taaswira ya kuwepo kwa mfumo wa uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu ya Tume hiyo, ikiwa ni pamoja na upokeaji wa taarifa, maoni na malalamiko ya wananchi kwa viongozi wao na watendaji ambao Tume inawasimamia.

Aidha, alisema kuwa ni vyema watumishi kushirikiana pamoja na viongozi wao ili kuhakikisha jamii inapata huduma bora hususan katika kuhakikisha maadili ya utendaji kazi hayakiukwi ikiwa kwa Viongozi wa Umma ama kwa watumishi wengine.

Sambamba na hayo Katibu, Jidawy amewataka wananchi kushirikiana na Tume katika kuimarisha maadili ya viongozi kwani amefafanua kuwa kiongozi bora ni lazima atokane na familia bora na malezi bora hivyo ni jukumu la kila mwanafamilia kuhakikisha inawalea watoto katika makuzi mema ili kuweza kupata viongozi bora.

Akiwasilisha rasimu ya mkataba wa utoaji huduma, Mwanasheria wa Tume hiyo, Makame Mussa Mwadini alisema kuwa Tume itaendelea na jitihada zake kwa kusimamia utekelezaji wa Sheria nambari 4 ya mwaka 2015 ikiwemo kusimamia maadili ya viongozi.

Aidha alisema, Tume hiyo inahakikisha inazingatia misingi ya usri katika utekelezaji wa majukumu yake ikiwa ni pamoja na kuhifadhi taarifa za Viongozi wa Umma na taarifa mbali mbali inazopokea toka kwa wananchi.

Sambamba na hayo, alisema kuwa ili kuhakikisha mkataba huu unaleta manufaa na kukidhi mahitaji ya wataka huduma ambapo mkataba huo utakuwa ni wa miaka mitatu kulingana na mabadiliko mbalimbali yanayotokea kulingana na wakati husika.

Hata hivyo, alisema kuwa mkataba huo, unalengo la kuainisha huduma, viwango vya utoaji huduma, kusisitiza umuhimu wa wataka huduma na taratibu za kulalamikia huduma pale ambapo mwananchi asiporidhishwa.

Nao washiriki wa mkutano huo, waliahidi kuyafanyia kazi masuala yote yaliyokuwemo kwenye rasimu hiyo yanayowahusu wananchi ili lengo lifikiwe na kuweza kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii juu ya viongozi wao.

Pamoja na hayo, waliishauri Tume, kuweza kuufanyia marekebisho mkataba huo kwa baadhi ya vipengele ili kuweza kuendana na mahitaji ya nchi na jamii ya kizanzibari.

Mkutano huo wa kujadili rasimu ya mkataba wa huduma kwa wateja uliwashirikisha baadhi ya watendaji mbali mbali wa Serikali na wasio wa Serikali wakiwemo masheha, madiwani, mahakimu, wakurugenzi, wahasibu, wajumbe kutoka taasisi binafsi na taasisi za kiraia.

Mkataba huo umetayarishwa kutokana na matakwa ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuzitaka taasisi zote za Serikali kutayarisha mikataba ya huduma kwa wateja ili kuweza kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

“FUATA MAADILI, TUIMARISHE UTAWALA BORA”