Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar

Maadili mema ni kichocheo cha maendeleo na Amani katika nchi

UADILIFU ni dhana moja ambayo kuielezea kwake hutaacha kuigusa dhana ya Utawala Bora. Kuitwa mtumishi ama kiongozi aliyetukuka mbali na sifa nyengine kunashabihiana sana na matendo ya uadilifu. Huwezi kuitwa kiongozi aliyetukuka kama kutakosekana uadilifu katika matendo yako.

Uadilifu ingawaje ni neno dogo lakini katika taaluma ya utawala na uongozi lina maana pana. Kwa kawaida unaweza kusema ni tabia ya mtu kuwa mkweli, muaminifu, muwazi, muwajibikaji na mtenda haki katika kutekeleza majukumu yake ya kazi.

Lakini tunapoiangalia maana ya tafsiri halisi kupitia kamusi mbali mbali za Kiswahili tunaelezwa kuwa ni hali ya mtu kufanya haki bila ya kuegemea upande mmoja. Hii inamaana ya kusema kuwa ni hali ya kukipa kila kitu kinavyostahiki, ikiwa ni nafsi, kitu ama jambo lolote lile.

Ni dhahiri kuwa dhana ya uadilifu imezungumziwa kupitia imani zote ikiwemo ya Uislamu na Ukristo. Ni kusema kuwa kama dini zote zimeweza kuzungumzia uadilifu ni dhahiri shahiri kuwa hata katika mienendo yetu na katika shughuli zetu hatuna budi kuifuata misingi ya uadilifu katika utendaji wa kazi zetu.

Vitabu vitakatifu vinatueleza kuwa msingi wa maisha ya binaadamu unatokana na dini anayoiamini na ni wazi kusema kuwa binaadamu hawezi kuishi bila ya dini na mafundisho ya dini zote zimehubiri kuhusu dhana ya uadilifu. Kama dini ya Uislamu inapolitambua hili kwa kusema hukumu ya uadilifu ni wajibu na ni fardhi katika uislamu kwa kila mtu, awe Muislamu au asiye Muislamu kama Mwenyezi Mungu anavyobainisha hayo. “Hakika Mwenyezi Mungu Anaamrisha uadilifu na ihsaan na kuwapa jamaa (na wengineo) na anakataza machafu, maovu na dhulma”. Hii inamaana kuwa uadilifu umehimizwa katika kauli, vitendo, ikiwa katika mahusiano ya mtu wa karibu au wa mbali ikiwa kwa rafiki au kwa adui ikiwa kwa kiongozi au waongozwaji ni wajibu kwa kila muislamu. Hivyo wale waliobahatika kuwa Viongozi wa Umma wanatakiwa kufuata misingi ya uadilifu.

Kwa hakika Mwenyezi Mungu anatuamrisha kuhukumu kwa kuzingatia uadilifu na anatukataza kufuata matamanio mabaya kwa kuitupa haki na kufuata hisia za upendeleo na chuki, na kuzingatia vigezo vya nasaba au hadhi ya kijamii katika kuwapendelea watu fulani, na hii ndiyo inayosababisha khiyana na uonevu.

Wakristo wanaaswa kupitia vitabu vyao “utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.” Hii nikwamba haki ndiyo inayoleta uadilifu na kufuata misingi ya uadilifu kunaleta neema nyingi nchini. Mafundisho yanatufundisha mengi tu ambayo hatuwezi kuyamaliza kuyasema kwake lakini Ukristo huo huo unatufundisha kuwa kila lisilo la haki ni dhambi, na dhambi isiyo ya mauti na kututaka tusiwe na tabia ya kupenda fedha; tuwe radhi na vitu tulivyonavyo.

Imebidi kuyaeleza haya kwani viongozi ni lazima tukumbushane kufuata misingi ya haki inayotokana na imani zetu na kutekeleza sheria, kanuni na taratibu zinazotuongoza katika utendaji wetu wa kazi kwani huku ndiko kukuza maadili yetu pamoja na uadilifu wetu.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanzisha Tume ya kusimamia maadili ya Viongozi wa Umma ili kuona Viongozi wa Umma hawatoki katika misingi ya uadilifu. Jina lake pekee linasadifu dhana ya uadilifu, hivyo ni vyema kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuanzisha Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Serikali imefanya haya kwa kuangalia faida kubwa inayopatikana katika kukuza uadilifu kama ilivyokwisha kubainishwa katika maandiko mbali mbali ya vitabu vitakatifu. Faida nyengine ni kuondoka kwa aina zote za dhulma, kuenea utulivu katika jamii, kuongezeka kwa upendo na uzalendo, kuaminiana, kuondoa rushwa katika jamii, kuondosha choyo, uhasidi, wivu, ujambazi, kuleta maendeleo na mengineyo.

Tunaelezwa kuwa dhana ya uadilifu huanza kutekelezwa tangu katika msingi wa familia ambapo hapa huweza kuenea baina ya mtu na mtu, familia na familia, kizazi hadi kizazi na kubakia katika zama. Na kama familia na jamii ndio chanzo cha uadilifu wa binaadamu na Serikali zetu nazo zimeweza kutambua kuwa ni sehemu ya taasisi muhimu kuweza kuuendeleza uadilifu wa binaadamu ama kuuanzisha uadilifu huo.

Misingi hii ya uadilifu ikifuatwa ipasavyo katika jamii dunia huweza kubaki sehemu salama kwani uadilifu hapa utaingia katika mawanda ya uongozi ambapo ndio kihakikisho tosha cha amani na usalama kwa wananchi katika nchi mbali mbali.

Elimu husaidia sana kuweza kumbadilisha binaadamu fikra na mtazamo alionao. Hivyo, ni wajibu wa kila mmoja wetu kwa nafasi yake ikiwa ni mtu na mtu, taasisi, vyuo, madrasa, skuli, taasisi binafsi, mashirika, vyama vya ushirika, taasisi zisizo za serikali na nyenginezo kusaidia kufikisha elimu ya maadili ili kuweza kutengeneza na kutayarisha wananchi wazalendo na viongozi bora katika ustawi wa maisha yetu na maendeleo ya nchi yetu.

Suala la kuimarisha misingi ya maadili halibaki kwa taasisi zenye dhamana ya kuimarisha utawala bora pekee, kwani athari za kuacha kutekeleza misingi ya maadili ni kihatarisho cha ustawi wa maisha ya binaadamu katika nchi yetu.

 “FUATA MAADILI, TUIMARISHE UTAWALA BORA”