The Revolutionary Government of Zanzibar

Wahariri watakiwa kuacha kufanya kazi kwa shinikizo na ushawishi

WAANDISHI wametakiwa kuyaibua matendo maovu yanayofanywa na viongozi wa umma ili kuiepusha jamii kukosa haki zao za msingi na kushamiri kwa rushwa katika jamii.

Afisa Uhusianao na Elimu wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma Zanzibar, ndugu Haji Juma Chapa ameyasema hayo wakati akiwasilisha mada ya Jukumu la Wahariri wa Vyombo vya Habari katika Kudumisha Maadili kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Umoja wa Watu Wenye Ulemavu uliopo Kikwajuni Mjini Unguja kwa Wahariri wa Vyombo vya Habari.

Alisema, “endapo Wahariri wa vyombo vya habari wataacha kutekeleza wajibu wao ipasavyo jamii itachelewa kupata maendeleo, rasilimali za nchi zitawafaidisha watu wachache, taasisi za Umma zitafanya kazi bila ya ufanisi, viongozi wa Umma watajilimbizikia mali isivyostahili, wananchi watakosa imani na Serikali na viongozi kutowajibika katika majukumu yao.”

Alifahamisha kuwa wahariri wanawajibu wa kushirikiana na Tume kwa kutoa taarifa za uvunjifu wa maadili unaofanywa na viongozi wa umma kwani matatizo mengi yanayoibuka katika jamii yanasababishwa na jamii kuacha kutekeleza wajibu wao ipasavyo hivyo kupelekea athari kutokea katika maeneo mengine.

“Wahariri wa habari pamoja na waandishi mnawajibu wa kuwashirikisha wananchi kwa ukamilifu katika kuvitumia vyombo vya habari, kuandaa ajenda, vipindi na kuweka muda/nafasi maalum ya kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuimarisha maadili”. Alisema ndugu, Chapa.

Aidha, wahariri wametakiwa kuvitumia vyombo vyao katika kukuza mila na desturi za kizanzibari, kushirikiana na Serikali katika kuendeleza yaliyo mema na kufuata na kudumisha maadili ya uhariri wa habari.

Amewataka wahariri kuacha kufanya kazi kwa kufuata shinikizo, ushawishi, ushabiki, kuchanganya na maslahi binafsi, ubaguzi kwani huko ni kukiuka miiko ya uhariri wa habari.

Akizungumzia juu ya umuhimu wa upatikanaji wa habari amesema kuwa jambo hilo sio anasa kuwepo katika jamii bali ni suala la muhimu sana na uhuru huo usichukuliwe kuwa ni jukumu la waandishi pekee kuweza kuwasilisha mawazo yao tu na kuandika bali lazima uhusishwe na jamii katika haki ya kuweza kupata elimu, kutoa taarifa na kubadilishana mawazo ili kuweza kukuza maendeleo na ustawi wa jamii.

Aidha, aliongezea kuwa licha ya uhuru huo kutambuliwa kwa mujibu wa Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Binaadamu wa mwaka 1948, Mkataba wa Afrika wa Haki za Binaadamu pamoja na kutambuliwa na Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984 uhuru huo umewekewa mipaka na kukiuka mipaka hiyo ni kuenda kinyume na maadili ya kazi ikiwa ni pamoja na waandishi wa habari.

Katika muwasilisho wake ndugu Chapa amesisitiza kuwa vyombo vya habari vina mchango mkubwa endapo vitatumika kwa mujibu wa malengo yaliyokusudiwa ikiwemo kuiweka jamii karibu na viongozi wao, kuibua maovu katika jamii, kusaidia jamii kuweza kutambua sifa za kiongozi bora na kuweza kufanya maamuzi sahihi wakati wa kuchagua wawakilishi wa wananchi. Aidha, huweza kusaidia kufahamu na kujifunza misingi ya demokrasia, husaidia viongozi kuweza kutekeleza wajibu wao na kuchangia maendeleo ya jamii.

Kwa upande wake Afisa Huduma za Sheria, Ndugu Makame Mussa Mwadini akiwasilisha mada ya Sheria ya Maadili amefahamisha kuwa Viongozi wa Umma wamewekewa misingi katika utendaji wa kazi zao ambayo wanapaswa kuwajibika nayo ikiwemo kujaza fomu ya Tamko la Mali na Madeni, kutangaza mgongano wa kimaslahi na kuzingatia miiko na maadili ya uongozi.

Amebainisha kuwa, kukiuka misingi ya maadili kwa Kiongozi wa Umma ikiwemo kulewa kupindukia, kujihusiha na uasherati, uropokwaji na utoaji wa siri za Ofisi, uzembe na kutojali matatizo ya wananchi, kushindwa kutunza familia na wazee wake ni miongoni mwa mambo yanayokatazwa kwa Kiongozi wa Umma. Hatahivyo, kushirikiana na watu wenye mienendo isiyokubalika, kushindwa kulipa madeni, kutumia kauli ama lugha isiyofaa na Ugomvi nako ni kukiuka maadili.

Aliongezea kuwa udhalilishaji wa kijinsia, vitendo vya jinai, utapeli, wizi, na ubakaji ni miongoni mwa mambo ambayo kiongozi wa umma hatakiwi kujihusisha nayo na endapo atajihusisha kwenye mambo hayo hatua za kinidhamu huchukuliwa kwa kiongozi wa umma ikiwemo kupewa onyo, kukatwa mshahara kushushwa cheo, kusimamishwa kazi, kushauriwa kustaafu, kuondolewa madarakani au hata kufukuzwa kazi.

Akitaja baadhi ya mambo yanayompelekea kiongozi wa umma kuvunja maadili kuwa ni matumizi mabaya ya taarifa, kutoa taarifa rasmi kwa asiyehusika, kutumia ushawishi katika uteuzi, upandishaji vyeo, kutoa adhabu au kumuondoa kazini mtumishi wa umma. Mengine ni kutumia mali ya Serikali kwa matumizi binafsi au matumizi yasiyoidhinishwa kwa nia ya kujipatia maslahi ya kiuchumi, kushindwa bila sababu ya msingi kutangaza mali na madeni, kutoa Tamko la Mali na Madeni lisilo la kweli au lenye kupotosha, kutumia wadhifa vibaya kwa faida yake au kwa jamaa zake na kukiuka kifungu chochote cha Sheria ya Maadili.

Sambamba na hayo, ndugu Mwadini aliwataka wananchi ikiwa pamoja na wahariri wa habari kutoa taarifa za uvunjwaji wa maadili ya viongozi wa umma na kutoa ushirikiano na msaada unaohitajika katika utekelezaji na usimamizi wa Sheria ya Maadili kwani ni wajibu wa kila mwananchi uliotambuliwa na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

“FUATA MAADILI, TUIMARISHE UTAWALA BORA”