The Revolutionary Government of Zanzibar

Kamati ya BLW yaridhishwa na utendaji wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma

Kamati ya Kudumu ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi imeelezea kuridhishwa na taarifa ya utekelezaji wa kazi za Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma katika kipindi cha Januari hadi Machi 2023, na kuitaka Tume hiyo kuendelea kufanyakazi kwa  uadilifu ili kuimarisha dhana ya Utawala bora nchini.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe, Machano Othman Said alieleza  hayo mara baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa kazi za Tume katika kikao kilichofanyika kwenye Ofisi za Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma Vuga.

Akizungumza katika kikao hicho Mhe. Machano alisema , Tume ya Maadili inajukumu kubwa la kusimamia nidhamu za Viongozi wa Umma waliopo katika taasisi za Serikali, hivyo ni vyema kwa watendaji wa Tume hiyo kuendelea kutunza siri za viongozi sambamba na kuhakikisha kuwa
viongozi wanafanyakazi kwa kuzingatia maadili ya uongozi yaliyowekwa kisheria.

Aidha Mhe. Machano aliutaka uongozi wa Tume hiyo kutosita kuwachukulia hatua za kinidhamu Viongozi wa Umma watakaobainika kuwabugudhi na kuwafanyia vitisho wafanyakazi katika taasisi za Serikali na wananchi wanaotoa taarifa za viongozi wanaovunja maadili ili kujenga mazingira mazuri kwa wananchi na kuendelea kutoa mashirikiano ya utoaji wa taarifa katika Tume hiyo .

Alifahamisha kuwa kiongozi wa umma chini ya sheria ya maadili ya viongozi
anatakiwa kuwa na misingi ya kimaadili wakati wote anapokuwa madarakani na kujiepusha na vitendo vinavyokwenda kinyume na sheria hiyo jambo ambalo watumishi wa umma na wananchi kwa ujumla wasingependa
kuyaona.

Akiwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa kazi za Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kaimu Katibu wa Tume hiyo ambae pia ni Mkurugenzi Mipango, Utawala na Rasilimali watu Ndugu, Haji Ramadhan Haji amesema, katika kipindi cha Januari hadi March 2023 Tume ya Maadili imafanikiwa kupokea,
kusajili na kuhifadhi fomu za Tamko la Mali na Madeni kwa Viongozi 27 sawa na asilimia 54 ya Shabaha ya Viongozi 50 iliyopangwa kwa kipindi hicho, ambapo kati ya hizo fomu 25 zilipokelewa Unguja na fomu 2 zilipokelewa kwa upande wa Pemba.

Alifahamisha kuwa katika kipindi hicho cha utekelezaji Tume imefanya uhakiki wa taarifa za mali na madeni kwa Viongozi wa Umma 66 wenye nyadhifa mbalimbali katika taasisi za Serikali wakiwemo Wakurugenzi , Maafisa Wadhamini, Makatibu Tawala, Mameneja, Makatibu wa bodi, Afisa Mtambuzi wa Ardhi na Wahasibu na kwamba  kati ya hao 49 kutoka Unguja na 17 kwa upande wa Pemba.

Akizungumzia kuhusu malamiko ya ukiukwaji waMaadili ya Viongozi wa Umma kutoka kwa wananchi Mkurugenzi Haji alieleza kuwa , Tume imepokea jumla ya malalamiko 5 yaliyohusisha matumizi mabaya ya madaraka na uonevu na kwamba kati ya malalamiko hayo 3 uchunguzi wake unaendelea na malalamiko 2 uchunguzi wake umekamilika .

Adha aliongeza kuwa, Tume baada ya kufanya uchunguzi na kuridhishwa na tuhuma zinazowasilishwa dhidi ya viongozi husika inaandaa ripoti ya maamuzi na kuiwasilisha kwenye mamlaka za kinidhamu zinazowasimamia Viongozi hao ili wachukuliwe hatua za kinidhamu kama sheria namba 4 ya mwaka 2015 ya Maadili ya Viongozi wa umma inavyoelekeza.

“Sisi Tume ya Maadili hatuwapeleki viongozi mahakamani kwa mujibu wa sheria yetu ya maadili ya viongozi, ripoti za maamuzi tunaziwasilisha kwenye mamlaka za uteuzi kwa hatua”alisisitiza.

Pamoja na mambo mengine Ndugu Haji alisema Tume ya Maadili inaendelea na jukumu lake la msingi la kutoka elimu kwa Viongozi, wafanyakazi katika taasisi za Serikali pamoja na wananchi na kwamba Tume inaendelea kuimarika katika utekelezajiwa majukumu yake kutokana na mashirikiano wanayoyapata kutoka kwa viongozi na wananchikwa ujumla.

Nae Mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya Viongoziwa Umma Ndugu Assaa Ahmad Rashid aliwaeleza wajumbe wa kamati hiyo kuwa, miungoni mwa
changamoto za utekelezaji wa kazi za Tume ni kuwepo kwa baadhi ya viongozi wa umma kuwafanyia vitisho wafanyakazi na wananchi wanaowasilisha
malalamiko ya ukiukwaji wa maadili ya viongozi wa Umma hali ambayo inaweza kuathiri utekelezaji wa majukumu ya Tume hiyo.